Blair ataka Afrika kusaidiwa zaidi

Tume iliyoundwa na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair kutafuta suluhisho juu ya hali ya umasikini barani Afrika imetoa wito wa pauni bilioni zaidi ili kulisaidia bara hilo.

Image caption Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza ataka misaada zaidi itolewe kwa mataifa ya Afrika

Taarifa iliyotolewa wakati mkutano wa kilele kukabiliana na umasikini duniani ukitarajiwa baadaye mwezi huu mjini New York, tume hiyo imesema kuwa bara linaloongoza kwa ufukara duniani limepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Hata hivyo taarifa hiyo imeongezea kusema kuwa bado juhudi za kupunguza umasikini zimepata changamoto kali za kuuondoa katika maeneo mengi ya Afrika.

Afrika, inasema taarifa hiyo, imebadilika vilivyo katika miaka mitano iliyopita.

Kumekuwepo kile taarifa hiyo ilichotaja kama mabadiliko katika kukua kwa uchumi, ongezeko la biashara na uwekezaji, siyo tu kutokana na kuwepo na haja ya mali asili kutoka mataifa kama China na India.

Hata hivyo, tume inasema kuwa idadi kubwa ya watu barani humo hawajapata faida ya ufanisi huu wa kukua kwa uchumi.

Halikadhalika mabadiliko katika mazingira na kupanda kwa bei ya chakula kunafanya vita dhidi ya umasikini kuzidi kuwa kigezo kikubwa ikilinganishwa na mafanikio kama idadi kubwa ya watoto kuweza kwenda shule na kulala katika vitanda vyenye vyandarua vya kukinga malaria.

Taarifa hiyo inadokeza, kwa mfano, kuwa idadi ya watoto wenye hali ya utapia mlo haijabadilika katika kipindi cha miaka ishirini.

Tume inasema kuwa kuomba msaada kwa wakati huu huenda kusipokelewe vizuri na mataifa wahisani ambayo yanapitia kipindi cha kupunguza matumizi ya fedha zake.

Ingawaje Tume hiyo inahimiza risala iliyokuwa kichwa cha taarifa yake ya mwaka 2005 kuwa Afrika iliyo imara, yenye maendeleo ni muhimu kwa kila mhusika.