Man United yavutwa shati na Bolton

Bolton na Manchester United
Image caption Bolton na Manchester United

Manchester United imeshindwa kutumia kutetereka vinara wa ligi Chelsea, wakati walipolazimishwa kwenda sare na Bolton ya kufungana mabao 2-2.

Bolton waliokuwa uwanja wa nyumbani, walikuwa wa kwanza kutikisa nyavu za Manchester United baada ya mlinzi Zat Knight kuunganisha mpira wa kona, kabla ya Nani kuisawazishia Man United baada ya kuwapangua wachezaji wa Bolton na kusawazisha bao hilo.

Lakini Martin Petrov alifufua matumaini ya ushindi baada ya kupachika bao zuri la pili kwa Bolton baada ya shuti lake kumchanganya beki wa Man United Darren Fletcher.

Michael Owen aliyeingia kipindi cha pili aliunganisha vizuri kwa kichwa mpira wa free-kick ulioihakikishia Man United bao la kusawazisha.

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson awali alisisitiza wangetumia mechi na Bolton kupunguza wigo wa pointi na Chelsea, ambao siku ya Jumamosi walifungwa bao 1-0 na Manchester City.

Hata hivyo Manchester United waliambulia pointi moja katika uwanja wa Bolton wa Reebok.

Kwa matokeo hayo Manchester United imefanikiwa kujisogeza hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi 12, wakiisukuma Arsenal nafasi ya tatu, huku Chelsea wakiendelea kung'ang'ania nafasi ya kwanza kwa pointi 15.