Messi aumizwa kutocheza wiki mbili

Lionel Mess ameumia kiwiko cha mguu wakati Barcelona ilipoilaza Atletico Madrid mabao 2-1 katika mchezo wa ligi ya Hispania maarufu La Liga.

Image caption Lionel Messi

Mshambuliaji huyo anayechezea pia timu ya taifa ya Argentina, alitolewa nje kwa machela kipindi cha pili baada ya kuchezewa rafu na mlinzi wa Atletico Tomas Ujfalusi na kuna uwezekano hatacheza soka kwa wiki mbili zijazo.

Taarifa rasmi ya Barca kupitia mtandao wa klabu hiyo imethibitisha Messia ameumia kiwiko cha mguu wa kuume, lakini hakuna mfupa uliovunjika.

Mchazaji huyo bora wa dunia wa mwaka anatazamiwa kufanyiwa vipimo Jumatatu kubainisha ukubwa wa kuumia kwake.

Licha ya Ujfalusi kuoneshwa kadi ya pili ya manjano kwa rafu hiyo, kocha wa Barcelona Pep Guardiola alimshutumu mwamuzi David Fernandez Borbalan.

Guardiola ameongeza kusema kimsingi, Messi hakuvunjika suala ambalo lilikuwa likiwapa mashaka. Baada ya vipimo watafahamu ukubwa wa tatizo.

Picha za televisheni zinajieleza. Si Cristiano Ronaldo pekee anayehitaji kulindwa, waamuzi wanahitajika kuwalinda wacheza wote.

Messi anatazamiwa kukosa michezo ya ligi dhidi ya Sporting Gijon, Real Mallorca na Athletic Bilbao pamoja na pambano la ubingwa wa Ulaya dhidi ya Rubin Kazan tarehe 29 mwezi wa Septemba.

Mshambuliaji huyo aliipatia bao la kuongoza katika dakika ya 13 katika uwanja wa Vicente Calderon, lakini Raul Garcia akasawazisha dakika 11 baadaye.

Mabingwa hao wa Hispania walikosa nafasi nyingi za kufunga kabla Gerard Pique kufanikiwa kuipatia bao la pili na kuzoa pointi zote tatu kwa shuti kali la karibu.