Wanariadha wa Uingereza wajitoa Madola

Uhuruogu, Idowu na Dobriskey
Image caption Uhuruogu, Idowu na Dobriskey

Wanariadha watatu wa Uingereza Phillips Idowu, Christine Ohuruogu na Lisa Dobriskey wamejitoa katika mashindano ya Jumuia ya Madola yatakayoanza tarehe 3 mwezi wa Oktoba mjini Delhi, India.

Bingwa wa dunia wa kuruka miruko mitatu Idowu amejitoa kutokana na wasiwasi na hali ya usalama kwa mashindano hayo, wakati Ohuru na Dobriskey wamejeruhiwa.

Wanariadha hao watatu walitarajiwa kutetea mataji yao ya Madola mjini Delhi.

Kujitoa kwa wanariadha hao kumekuja wakati kumetanda tuhuma zilizoelekezwa kwa waandaaji wa mashindano hayo kwamba kijiji cha wanariadha hakifai binadamu kuishi.

Kupitia mtandao, Idowu amewataka radhi wapenzi wa riadha, lakini akasema anao watoto inaombidi awafikirie. Alisema usalama wake ni muhimu zaidi ya medali.

Ameongeza kusema watu watakuwa wamekatishwa tamaa na uamuzi wake, lakini kutokana na hali halisi ya usalama hawezi kushiriki na hata yeye amekatishwa tamaa sana.

Ohuruogu, bingwa wa Olympiki wa mbio za mita 400, amesema asingependa kujiumiza zaidi msuli wake baada ya kuumia wakati wa mazoezi.

Dobriskey, aliyeshinda mbio za mita 1500 katika mashindano ya Madola ya mwaka 2006 mjini Melbourne, lakini kwa sasa anasumbuliwa na maumivu ya mguu.