Kifo cha panda wa China chachunguzwa

Panda
Image caption Panda

Kundi la wataalamu kutoka Uchina limewasili Japan kupeleleza kifo cha panda aliyekopwa kutoka Uchina.

Mnyama huyo alifariki wiki iliyopita kutokana na mshituko akiwa kwenye hifadhi ya wanyama ya huko Kobe. Wakuu wa Uchina huenda wakadai fidia ya hadi dola 500,000.

Panda hawa wakubwa labda ndiyo maarufu kutumwa nje kutoka Uchina, na wakuu wa Uchina wanamuona mnyama huyo kuwa ni mwenye thamani kubwa.

Kwa hiyo kutokana na kifo cha Co,(jina la mnyama huyo) mwenye umri wa miaka 14 ndani ya hifadhi huko Japan kwa mshituko wa moyo baada ya kudungwa sindano ya kupooza imebidi wakuu wa Uchina kutuma wataalamu wake kupeleleza kifo hicho.

Gazeti moja limedai kuwa panda huyo CO alikufa kwa kudungwa sindano ya kumpooza ili wavute manii yake wakiwa na mpango wa kuzalisha panda wao wenyewe.

Panda hawa wakubwa ni miongoni mwa wanyama adimu duniani walio kwenye orodha ya wanyama walio hatarini kutoweka.

Halikadhalika, hawa ni wanyama wasiopenda kushika mimba wakiwa nje ya makaazi yao asilia.

Shirika moja la Uchina linaloshughulikia wanyama pori, limesema kuwa chini ya mapatano ya mkopo, hifadhi ya wanyama ya Japan sharti ilipe fidia kufuatia kifo hicho.

Bado haijabainika kama wakuu wa Uchina wataishinikiza Japan ilipe fidia.

Kifo cha CO kinatokea wakati kuna mvutano baina ya nchi hizo mbili juu ya visiwa vinavyozozaniwa vilivyoko mashariki mwa bahari ya Uchina.

Japan inawashikilia wavuvi wa Kichina baada ya boti lao kugongana na maboti mawili ya walinzi wa Kijapani karibu na visiwa hivyo.

Uchina imeonya kuwa Japan inawajibika juu ya tukio hilo na kuitaka imuachilie nahodha wa boti la wavuvi haraka iwezekanavyo.