Ghana kupunguza umaskini 2015

Ghana
Image caption Ghana

Viongozi wa mataifa mbalimbali duniani wanakutana kwenye Umoja wa Mataifa wiki ijayo kutathmini maendeleo yaliyofikiwa katika malengo ya milenia.

Wakati viongozi wakijiandaa kwa mkutano huo taasisi moja ya Uingereza inayohushughulika na masuala ya maendeleo ya kimataifa, Overseas Development Institute imechapisha takwimu yake kuhusu mchango wa jitihada za chombo kinachopania malengo hayo yatekelezwe. Malengo ya Milenia yalianzishwa na viongozi wa dunia miaka kumi iliyopita kama njia ya kupima viwango vya maendeleo ya kufikia kupunguza umasikini ifikapo mwaka 2015.

Lakini kumekuwepo na mashaka kama juhudi hizi zimefanikishwa, kwa sababu mengi hayajafikiwa, hususan barani Afrika.

Ingawaje taarifa hii ya taasisi ya maendeleo ya kimataifa inaonyesha kuna sababu ya kuwa na matumaini, kutokana na ushahidi kutoka katika maeneo ambako maendeleo yameonekana.

Mmoja wa wahariri wa taarifa hii, Claire Melamed -alisema "Kabla ya hapa tulitegemea msaada wa kimataifa kuchangia katika kuleta maendeleo haya. Lakini la muhimu ni yanayofanyika ndani ya nchi, shughuli za watu wake kuweza kukabiliana na umasikini na kupata sera muafaka kwao kupambana na tatizo la umasikini."

Ghana yaimarika

Mojawapo ya nchi zilizotajwa kama zilizofanikisha mpango huo ni Ghana, ambako kilimo kimeonyesha kuimarika, kikikua kwa zaidi ya asilimia tano kwa kila mwaka.

Kukua huko kumezua soko la kuvutia wakulima wazawa na kuwazidishia mapato. Hivyo, siri ya Ghana iko wapi?

Kwa mujibu wa taasisi ya Uingereza inayoshughulikia suala la maendeleo duniani ni mhimizo wake juu ya kilimo, sekta ambayo hupuuzwa na wahisani pamoja na serikali.

Kutokana na mabadiliko hayo ujenzi wa barabara na mpango wa kuendelea kuwekeza, yamechangia kuimarisha sekta ya kilimo katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.

Vipato vya mashambani vimepanda na umasikini umepungua. Utapiamlo miongoni mwa watoto umepungua kwa nusu.

Haya ni matokeo ya kuridhisha kutoka bara ambalo lina sifa kubwa ya kushindwa kutimiza ahadi zake na kuvunja matumaini yote.

Na sasa kwa sababu Ghana ina mafuta ya petroli, swali ni kama mtazamo wake juu ya kuendeleza kilimo utabadilika au utahimizwa.