Papa Benedikt XVI azuru Uingereza

Image caption Papa Benedikt Kuanza ziara Uingereza

Papa Benedict kwanza atafanya mkutano wa faragha na malkia Elizabeth. Baadaye atajiunga na mamia ya wakatoliki katika barabara za Edinburgh. Ziara yake hata hivyo inafanyika wakati ambapo kanisa katoliki linakabiliwa na kashfa nyingi, kuu ikiwa ile ya makasisi wake kuwanajisi watoto.

Makao makuu ya kanisa katoliki mjini Roma Italia, yanasema ziara ya Papa Benedict inanuiwa kuhimiza kurejea kwa maadili ya kikristo ambayo yamepuuzwa sana nchini humo. Idadi kubwa ya raia wa Uingereza wamejitenga na dini na hata imani kuhusu kuwepo kwa Mungu.

Mtafaruku

Lakini kanisa katoliki limelaumiwa kwa kuchangia katika kuwasukuma wengi kutoka kwa dini. Tayari ziara ya Papa Benedict inapingwa na wale ambao wamekerwa na visa vilivyoripotiwa vya unajisi wa watoto na makasisi wa kikatoliki. Kanisa hilo limelaumiwa kwa kutowafichua makasisi hao ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Pia kumekuwa na mjadala kuhusu kuruhusiwa kwa makasisi wa kikatoliki kuoa kutokana na shutuma zinazowakabili baadhi yao za kuwa na wapenzi wa siri.

Kwa ujumla idadi ya waingereza walio waumini wa kanisa katoliki imepungua mno na katika makanisa mengi wanaohudhuria ni wahamiaji.

Kutokana na hali hiyo, inaelekea kuwa idadi kubwa ya wale ambao Papa Benedict atakutana nao watakuwa watu wa asili mbalimbali zaidi, kuliko ilivyokuwa wakati wa ziara ya mtangulizi wake, John Paul wa pili mnamo mwaka 82.

Maandalizi

Serikali ya Uingereza imesema itaimarisha usalama wakati wa ziara ya Papa Benedict kwa hofu kuwa baadhi ya makundi yanayopinga ziara hiyo huenda yakajaribu kuzua vurugu. Mamia ya watu wanatazamiwa kufanya maandamano katikati mwa jiji la London hapo Jumamosi kupinga ziara hiyo.

Baadhi yao wameelezea kukerwa na bajeti ya zaidi ya dola milioni 12 ambazo zitatumiwa.