Uchaguzi wa ubunge wakamilika Afghanistan

Raia wa Afghanistan Wakipiga Kura
Image caption Raia wa Afghanistan Wakipiga Kura

Umoja wa Mataifa na wanajeshi wa muungano wa NATO nchini Afghanistan, wameafiki hatua ya raia wa nchi hiyo wa kuendelea na uchaguzi wa ubunge licha ya ghasia zilizosababisha vifo vya watu 14.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, amewapongeza wapiga kura nchini humo kwa ujasiri wao kufuatia vitisho hivyo kutoka kwa wapiganaji wa Taleban.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Staffan De Mistura, amesema ni mapema kutangaza kuwa uchaguzi huo umefanikiwa.

Kamanda mkuu wa majeshi ya muungano wa NATO, Generali David Patraeus, amesema uchaguzi huo umeonyesha kuwa hatma ya taifa hilo siku zijazo, imo mikononi mwa raia wake na wala sio chini ya wapiganaji au makundi yenye misimamo mikali.

Kwa mujibu wa takwimu za mwanzo, asilimia 40 ya wapiga kura walishiriki kwenye uchaguzi huo na matokeo yake yanatarajiwa kutangazwa mwisho wa mwezi ujao.