Megrahi atembelewa na baba wa mwathirika

Image caption Dr Jim Swire

Baba wa mmoja wa walioathirika na bomu la Lockerbie amekwenda Libya kumtembelea mtu pekee aliyetiwa hatiani kwa ukatili.

Dr Jim Swire alitumia kama saa moja kuzungumza na Abdelbasset Ali al-Megrahi katika hospitali huko Tripoli wiki iliyopita.

Dr Swire alimpoteza binti yake mwenye umri wa miaka 24, aitwaye Flora, katika bomu hilo la mwaka 1988, lakini anaamini Megrahi hana hatia na anataka uchunguzi upya.

Alisema raia huyo wa Libya, ambaye ana saratani ya tezi kibofu, anaonekana mzima kuliko alivyotarajia.

Megrahi aliachiwa huru kutoka gereza la Greencock kwa misingi ya kumwonea huruma mwaka jana.

Megrahi alimwalika Dr Swire wakutane.

Watu hao wawili mara ya mwisho walikutana Desemba 2008 wakati Dr Swire alipomtembelea katika gereza la Greenock.

Akizungumzia kuhusu mkutano wao huko Libya: "Niliridhika sana kumwona na kuona hali yake."

"Anaumwa sana lakini anaweza kutoka kitandani na kutembea, japo si kipande kirefu."

Megrahi alipewa kifungo cha maisha kwa kuhusika na mlipuko wa bomu katika ndege ya Pan Am 103 uliotokea kwenye mpaka wa Scotland.

Alipewa fursa ya kusafisha jina lake baada ya tume ya kuangalia upya kesi za jinai za Scotland (SCCRC) na kusema kuna sababu sita ambapo inaamini haki haikutendeka sawasawa.