ICG yaonya: Eritrea 'kushindikana'

Shirika moja la kimarekani limeonya kuwa Eritrea huenda likawa taifa lililoshindikana iwapo jumuiya ya kimataifa haitajihusisha na taifa hilo lililopo katika Pembe ya Afrika.

Image caption Rais Isaias Afewerki wa Eritrea

Shirika hilo - International Crisis Group - limesema Eritrea iko katika hali mbara, huku uchumi wake ukididimia kwa kasi.

Hii ni hali mbaya kuonekana, ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita, ambapo eritrea ilikuwa na changamoto lakini ilikuwa katika hali ya kawaida, limesema shirika hilo.

Eritrea ilipata ilipata uhuru wake mwaka 1993, ingawa pia inakabiliwa na vikwazo kutoka kwa Umoja wa Mataifa kwa tuhuma za kusaidia waasi nchini Somalia.

Nchi hiyo ilisitisha uanachama wake kwa Umoja wa Afrika kama hatua ya kupinga hatua hiyo, na hivyo imezidi kutengwa.

Utawala wa kimabavu

Eritrea imepigana vita mara mbili tangu ipate uhuru wake, ikiwemo vita dhidi ya kugombea mpaka na Ethiopia ambapo watu takriban 80,000 waliuawa.

Mark Schneider wa shirika la ICG anasema, ikiwa mambo yataendelea kama yalivyo sasa, hali ya Eritrea 'inakaribia kulipuka' huku utawala wa kimabavu wa Rais Isaias Afewerki ikikabiliwa na shutuma mbalimbali.

Image caption Ramani ya Eritrea

"Kuna mgawanyiko katika jeshi, na hali ya kutoridhika miongoni mwa idadi kubwa ya wananchi," amesema Mark, akizungumza na kipindi cha Network Africa cha BBC.

Hali hiyo imeonekana kwa idadi kubwa ya watu kuondoka nchini humo kama wakimbizi, na pia kuwepo na dalili ya kutoelewana wenyewe kwa wenyewe ndani ya nchi, amesema Bw. Mark.

"Si rahisi kwamba hali ya uimara iliyotokana na utawala wa mabavu katika siku za nyuma inaweza kuendelea kuwepo."

Ripoti hiyo inaonya kuwa jeshi la kujenga taifa, ambalo nia yake ni kujenga na kuleta maendeleo nchini humo, huenda ndio chachu ya kuuangusha utawala wa nchi.

Eritrea inahitaji msaada kutoka nje kwa misingi ya kuelewa zaidi masaibu ya nchi hiyo, imesema ripiti ya ICG.