Rwanda yaahidi kushirikiana na Umoja wa Mataifa

Ramani ya Rwanda

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amempongeza rais wa Rwanda Paul Kagame kwa kubadilisha msimamo wa awali kuwaondoa wanajeshi wake kushiriki katika shughuli ya amani ya Umoja wa Mataifa huko Darfur, Sudan.

Rwanda ilitishia kusimamisha ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa mwezi jana kufuatia ripoti iliyofichuka ambapo jeshi la nchi hiyo lilituhumiwa kutekeleza uhalifu wa kivita katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema kwenye kikao kilichofanyika pembezoni mwa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa, rais Kagame alijadili kuhusu ripoti hiyo inayotarajiwa kutolewa mwezi ujao na na katibu Mkuu Ban Ki Moon.

Ripoti hiyo imenadi visa 600 vya dhuluma dhidi ya binadamu vilivyotekelezwa katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kati ya mwaka 1993 na 2003.