Rooney kutocheza mechi ya Valencia

Wayne Rooney
Image caption Wayne Rooney

Wayne Rooney hatasafiri na kikosi cha timu yake ya Manchester United siku ya Jumatano kwa ajili ya mchezo ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Valencia, kutokana na kuumia kiwiko cha mguu.

Manchester United ilikuwa na matumaini mshambuliaji huyo atakuwa imara kucheza mechi hiyo katika uwanja wa Mestalla.

Lakini Rooney aliyebadilishwa siku ya Jumapili Man United walipotoka sare ya kufungana mabao 2-2 na Bolton, sasa ameungana na Ryan Giggs katika orodha ya majeruhi.

Giggs anakabiliwa na maumivu ya paja, hali itakayomfanya asicheze soka kwa wiki mbili zijazo.

Meneja msaidiza wa Man United Mike Phelan alisema baada ya mechi na Bolton Rooney angekuwa tayari kwa ajili ya pambano la ligi ya Mabingwa wa Ulaya, lakini vipimo alivyofanyiwa vimeonesha hawezi kucheza.

Manchester United ambao walianza heka heka za ligi ya Mabingwa wa Ulaya katika kundi lao la C kwa kwenda sare ya kutofungana na Rangers, itaikabili Valencia ambayo kwa sasa inaongoza ligi ya Hispania.

Valencia walianza kampeni ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwa kuichakaza Bursaspor ya Uturuki mabao 4-0.

Msimu huu Rooney bado hajaonesha makali, hali iliyomfanya meneja wake Sir Alex Ferguson akiri mchezaji wake huyo hajisikii vizuri kutokana na kuandikwa na kutangazwa sana na vyombo vya habari baada ya tuhuma zilizohusu maisha yake binafsi.