Sudan yachelewesha uandikishwaji wa kura

Image caption Sudan

Sudan imechelewesha uandikishwaji wa wapiga kura kwa ajili ya kura ya maoni ya Januari ya kuamua iwapo upande wa kusini ujitenge mpaka mwezi Novemba, wakionyesha wasiwasi juu ya ratiba.

Mwenyekiti wa tume ya kura hiyo alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kuruhusu mafunzo ya wafanyakazi na uwasilishaji wa makaratasi ya kupigia kura.

Aliyekuwa Rais wa Tanzania Benjamin Mkapa, aliyeteuliwa na Umoja wa Mataifa kusimamia mchakato wa kura hizo, aliiambia BBC bado kuna changamoto nyingi.

Lakini alisema kama vyama vyote viko radhi, ratiba itafanyika kama ilivyopangwa.

Kura ya maoni ni sehemu ya makubaliano ya amani ya mwaka 2005 ya kumaliza miongo miwili ya mgogoro baina ya upande wa kaskazini na upande wa kusini wenye utajiri wa mafuta ambapo takriban watu milioni 1.5 walifariki dunia.

Wachambuzi wanahofia kuna hatari ya mgogoro huo kuanza upya iwapo raia wa upande wa Kusini wakihisi Khartoum inajaribu kuchelewesha au kuvuruga kura upande wa kusini- miongoni mwa maeneo maskini duniani.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Muhammed Ibrahim Khalil, alisema uandikishwaji ulicheleweshwa kwa wiki tatu hadi Novemba 15.

Kulingana na shirika la habari la Reuters, fomu za uandikishwaji bado hazijawasili kutoka Afrika Kusini- na hazitarajiwi kufika hadi Oktoba mwishoni.

Bw Mkapa aliteuliwa wiki iliyopita na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuongoza jopo maalum la waangalizi kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa salama.

Akihojiwa BBC iwapo atathubutu kuchelewesha kura hiyo ya maoni kama maandalizi hayakukamilika, Bw Mkapa alisema: "Tutakabiliana na hilo, muda utakapofika."

"Lakini kwa sasa naona wajibu wetu ni kuhakikisha inafanyika tarehe 9 Januari."