Ecuador: Rafael Correa bado ni rais!

Image caption Rais Rafael Correa wa Ecuador

Rais Rafael Correa wa Ecuador ameruhusiwa kutoka hospitalini katika mji mkuu wa Quito alikokimbilia kujificha baada ya kushambuliwa kwa gesi ya kutoa machozi na maafisa wa polisi waliokuwa wakiandamana.

Jeshi la nchi lilitumia nguvu kumuokoa rais huyo, na ufyatulianaji wa risasi ulifuatia. Rais huyo alikaribishwa kwa shangwe nje ya kasri lake alikohutubia watu. Aliwaambia kuwa mtu mmoja amethibitishwa kufariki katika tukio hilo na kuitaja siku hii kama siku ya huzuni kwa nchi hiyo.

Image caption machafuko ya maandamano

Awali rais huyo alitangaza hali ya tahadhari baada ya polisi hao kuteka uwanja wa ndege na maeneo mengine ya mji wakilalamikia hatua ya rais kupunguza gharama ya marupurupu yao.

Makamanda wakuu wa jeshi la Ecuador wametangaza kumuunga mkono rais Correa.

Hisani

Wakati huo huo, muungano wamataifa ya America UNASUR, uliitisha mkutano wa dharura katika mji mkuu wa Argentina Buenos Aries ambapo wametangaza kumuunga mkono rais Correa.

Rais wa Peru Alan Garcia amesema kuwa ni jambo la aibu kuwa maafisa wa polisi walijaribu kutumia nguvu kuhujumu uongozi wa kidemokrasia. Amesema kuwa muungano huo utafanya kila juhudi kuimarish auongozi wa rais Correa.

UNASUR imesema kuwa Amerika haitakubali serikali za kidemokrasia kuvunjwa na watu wachache wanaotetea maslahi zao za kibinafsi.