Capello avutiwa na Kevin Davies

Meneja wa timu ya England Fabio Capello amemuita katika kikosi chake kinachojinoa kuikabili Montenegro, mshambuliaji wa Bolton ambaye hajawahi kuichezea timu ya taifa Kevin Davies.

Image caption Kevin Davies

Pambano hili litafanyika katika uwanja wa Wembley siku ya Jumanne tarehe12 mwezi huu wa Oktoba.

Davies, mwenye umri wa miaka 33, anaungana na Wayne Rooney, ambaye amepona maumivu ya kiwiko cha mguu, pamoja na washambuliaji wengine Darren Bent na Peter Crouch.

Pia wengine ambao Capello amewajumisha katika kikosi hicho ni pamoja na John Terry, Rio Ferdinand, Joe Cole, Aaron Lennon na mlinda mlango Rob Green.

Kiungo wa Arsenal Jack Wilshere amechaguliwa katika vikosi vyote viwili, cha wakubwa na walio na umri wa chini ya miaka 21.

England imeanza vizuri hekaheka za kuwania kufuzu mashindano ya Euro 2012 baada ya kuzifunga Bulgaria na Switzerland.

Kujumuishwa kwa Davies inatokana na kuumia kwa mshambuliaji wa Fulham Bobby Zamora na Gabriel Agbonlahor wa Aston Villa, huku mashabiki wakiona Capello amemsahau mshambuliaji wa Newcastle United Andy Carroll ambaye alishaoneshwa isara ya kuchaguliwa katika kikosi hicho.