Mashindano ya Jumuiya ya Madola yaanza

Mashindano ya 19 ya Jumuia ya madola yaliyoanza jana kwa kishindo mjini Delhi hii leo yameelekea viwanjani.

Kishindo cha kwanza kwa wanariadha kilikuwa ndani ya mabwawa ambapo waogeleaji kutoka Afrika mashariki walishiriki vilivyo.

Mkenya Shah Akshay Milan alishiriki mbio za mchujo wa mita 50 kuogelea kinyumenyume na kumaliza katika muda mzuri.

Image caption Mashindani ya Jumuiya ya Madola New Delhi, India

Mbio za wanawake butterfly mita 50, Kenya ilikuwa na Hanika Ajaykum Patel pamoja na Ilako Kanyali , Foum Mariam Muhammad Ali akaiwakilisha Tanzania.

Kwa bahati mbaya waogeleaji wote hao hawakuweza kutimiza muda unaotakiwa kufuzu halikadhalika Bruni Ehner Sylvie Tanya Atieno.

Baada ya mbio hizo Atieno alisema amesikitishwa na kushindwa kufuzu kwa hatua ya pili.

Mwingine aliyejiunga katika mkumbo huo alikuwa Jamila Lunkuse kutoka Uganda ambaye alimaliza mbali na waogeleaji wakali kutoka Canada na Australia waliomzidi kwa karibu dakika nzima.

Katika uwanja wa mchezo wa Squash zogo lilimzunguka binti mdogo mwenye umri wa miaka kumi na minne Kalinja Vimji aliyeonyesha kipaji chake kwa kuudunda mpira wa Squash.

Baba yake alisema bado anahitaji muda kufikia viwango vya wale anaoshindana nao.

Kwingine utaratibu wa kuonana na wakuu pamoja na wanariadha ndani ya kijiji chao umebadilika kwa waandishi wa habari wanaotaka kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa kiongozi wa msafara wa Kenya Steven Soyi, inabidi mwandishi atume ombi lake saa 24 kabla ya kutembelea kijiji wanakolala wanariadha.

Kero zinazowakumba waandishi wa habari zimekithiri ingawa wamejidhatiti kuona kila linalopita linawafika wasomaji na wasikilizaji wao.