Aliyemrushia mawe Rais Kabila 'ajiua'

Image caption Msafara wa Joseph Kabila

Ndugu na wanaharakati wamekataa kukubaliana na taarifa kuwa mtu mmoja aliyekamatwa kwa kurusha mawe kwenye msafara wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila alijiua.

Armand Tungulu Mudiandambu, raia wa Ubelgiji, alikutwa amekufa katika chumba cha gereza siku ya Jumamosi baada ya kukamatwa kwake wiki iliyopita na walinzi wa Rais mjini Kinshasa.

Maafisa walisema Bw Tungulu alionekana kama alijiua kwa kutumia foronya.

Lakini mwanaharakati wa haki za binadamu alisema hakuna mito kwenye magereza ya Congo.

Ofisi ya mkuu wa mwendesha mashtaka alisema uchunguzi rasmi ulifunguliwa lakini wanaharakati wanasema lazima ifanywe na wataalamu wa kujitegemea.

Mmoja wa ndugu wa Bw Tungulu aliiambia redio Ufaransa kuwa haamini Bw Tungulu alijiua.

Huku Jacob Baluishi wa Waangalizi wa Haki za Binadamu wa Congo akiiambia shirika la habari la AFP: " Hatuwezi kuelewa ni vipi mtu anaweza kujiua na foronya wakati sote tunajua hakuna mito kwenye magereza ya Congo."

Mwezi Juni, mwanaharakati mkuu wa haki za binadamu nchini Congo Floribert Chebeya alikutwa amefariki dunia baada ya kuitwa kwenye mkutano na mkuu wa polisi.