Kiongozi wa upinzani wa Ethiopia aachiwa

Image caption Birtuka Mideksa

Kiongozi wa upinzani wa Ethiopia Birtukan Mideksa ameachiliwa huru.

Kuachiwa kwake kumefanyika miezi minne baada ya ushindi wa kishindo wa serikali ya nchi hiyo katika uchaguzi mkuu.

Alikuwa mmoja miongoni mwa viongozi wa upinzani kufungwa maisha baada ya uchaguzi wa mwaka 2005.

Baadae walisamehewa, lakini Bi Birtukan alikamatwa tena kwa kukiuka sheria za kuachiwa huru.

Aliiambia BBC akiwa nyumbani kwake kwenye mji mkuu, ambapo kulikuwa na mkusanyiko wa watu wengi waliomlaki, "Nimefurahishwa sana."

Bi Birtukan mwenye umri wa miaka 36 alisema aliachiliwa huru kwasababu aliomba kusamehewa.

Alisema, "Jela ni sehemu mbaya sana, hasa kwangu mimi ambapo nilikaa peke yangu."

"Sasa niko huru, Nimerudi kwa binti yangu na familia yangu, nimefurahi mno."

Mwandishi wa BBC wa Addis Ababa Uduak Amimo alisema mamia ya wafuasi walianza kumshangilia na kuimba alipowasili nyumbani kwake akiambatana na mama yake na mwanawe.

Bi Birtukan aliwahi kuwa jaji na alikuwa miongoni mwa viongozi wenye umri mdogo na wenye mvuto zaidi wa muungano wa upinzani ambao walifanya vizuri dhidi ya chama tawala katika uchaguzi wa mwaka 2005.

Meles Zenawi siku ya Jumatatu aliapishwa kwa mara ya nne kwa kipindi cha miaka mitano kama waziri mkuu, kufuatia ushindi mzito mwezi Mei.

Lakini Umoja wa Ulaya na waangalizi kutoka Marekani walisema haikufikia viwango vya kimataifa.