Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na salim Kikeke

Wachimbaji na namba 33

Katika tukio la kunasa na kuokolewa kwa wachimbaji nchini Chile, kuna mambo ambayo yameoneakana na kuhusishwa na sakata zima. Kulikuwa na wachimbaji thelathini na watatu walionasa, ilichukua siku thelathini na tatu kuchimba na kuwafikia.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, watu wengine wanasema imetokea tu, lakini wengine wanasema, hata kuna kitu hapa. "Kazi ya kuchimba ilichukua siku thelathini na tatu, siku moja ya kila mmoja" amesema Mikhail Proestakis, meneja wa kampuni iliyochimba shimo la kuwaokoa. Shimo hilo lilikuwana upana wa diamita sitini na sita, ambayo ni thelathini na tatu mara mbili.

" Ninaamini masuala ya namba, lazima ina maana" amesema Mikhail.

Shughuli ya kuwaokoa wachimbaji hao ilianza Oktoba kumi na tatu, ambapo tarehe hiyo ikiandikwa kwa namba inasomeka kama kumi na tatu, kumi, kumi -- yaani tarehe kumi na tatu, mwezi wa kumi mwaka elfu mbili na kumi. Ukijumlisha kumi na tatu, na kumi na kumi, jawabu ni thelathini na tatu.

Jambo hilo alilisema hata rais wa Chile Sebastian Pinera. "Hii namba thelathini na tatu inatokea kila mahala, yaani ni miujiza" amesema Maria Segovia, dada wa mmoja wa wachimbaji walionasa. Aidha waumini kadhaa wa Kikatoliki walisema Yesu alikuwa na umri wa miaka thelathini na tatu wakati alipotundikwa msalabani.

Na wengine wamesema ujumbe wa kwanza wa maandishi uliotumwa na wachimbaji hao kuonesha kuwa bado wako hai ulikuwa na herufi thelathini na tatu. Ujumbe huo ulisomeka hivi "estamos bien en el refugio los 33".

08.08.08, 09.09.09 na 10.10.10

Mama mmoja nchini Marekani inaonekana hatukuwa na tabu sana ya kukumbuka tarehe za kuzaliwa za watoto wake watatu, kwani mmoja alizaliwa tarehe nane mwezi wa nane mwaka 2008, mwingine tarehe tisa mwezi wa tisa mwaka 2009, na mwingine tarehe kumi mwezi wa kumi mwaka 2010.

Gazeti la USA Today limesema mwanamama huyo wa Rockford Michigan pamoja na mumewe wala hawakuwa au kupanga wakifikiria kinachotokea. Mama huyo amesema baada ya kupata mtoto wa kwanza wa kike, hawakuwa wamepanga kupata wa pili. Hata hivyo alivyopata uja uzito madaktari walikadiria kuwa angejifungua tarehe ishirini mwezi wa tisa mwaka 2009, lakini kwa bahati mbaya, au nzuri mama huyo alipata matatizo kidogo ya uzazi na kulazimika kujifungua mapema kabla ya tarehe aliyotarajia, tisa mwezi wa tisa 2009. Wakapata tena mtoto wa kike.

Mama huyo amesema mumewe baada ya kuona wanae wawili wamezaliwa katika tarehe kama hizo, akamuambia mkewe tukipata wa tatu itakuwa vizuri iwapo naye tarehe zitakaa kama za ndugu zake. Hata hivyo uja uzito wa mtoto wa tatu ulivyopatikana, madaktari wakamuambia atajifungua Novemba 4 mwaka huu. Kwa mara nyingine tena mama huyo akapata tatizo dogo la uzazi na mtto wao wa tatu, ambaye ni wa kiume kuzaliwa tarehekumi mwezi wa kumi mwaka 2010.

Hata hivyo mwanamama huyo amesema, hawana mpango wowote wa kupata tena mtoto...

Dawa ya fedha

Raia wawili wa Cameroon wameingia matatani nchini Urusi, baada ya kuwaambia watu kuwa wanaweza kutumia uchawi kuzalisha fedha.

Wawili hao walichukua dola elfu thelathini na tano kutoka kwa wahamiaji wawili kutoka Tajikistan, na kuwambia kuwa wanaweza kutumia uchawi kuzifanya fedha hizo kuongezeka mara tatu.

Polisi wa Urusi wamesema juzi Alhamisi kuwa wamawashikilia wanaume wawili waliowatapeli wahamiaji kutoka Tajik mjini Moscow, kwa kuwaahidi kuzidisha fedha kwa kutumia mazingaombwe. "waliahidi kubadili dola elfu thelathini na tano kuwa dola laki moja na tano kwa kutumia nguvu za giza" kimesema chanzo cha kipolisi, kikikaririwa na shirika la habari la Interfax.

Katika tukio jingine linalofanana na hilo, mwezi Februari mwaka huu raia wawili wengine kutoka Cameroon walikamatwa katika mkoa wa Altai, Siberia, huko huko Urusi kwa kosa la kuuza dawa ambayo ikipakwa kwenye noti, fedha hizo zinajizidisha zenyewe.

Wabunge wa Urusi mwezi huu wameunga mkono muswada wa kubadili sheria za mazingaombwe. Sheria mpya itapiga marufuku utangazaji wa shughuli za mazingaombwe na waganga kwenye TV, na kuwataka wawe na leseni.

Nguruwe kulipa deni

Tukisalia huko huko Urusi, mama mmoja amenyanganywa nguruwe wake ili akauzwe kulipia deni analodaiwa mama huyo na benki.

Shirika la habari la Reuters limesema maafisa wa mahakama mashariki mwa Urusi walikakamata katoto ka nguruwe ka mama huyo, ambaye anadaiwa na benki Roubles elfu kumi na tatu, sawa na dola mia nne na thelathini na mbili. Maafisa hao wamesema juzi alhamisi kuwa watakauza katoto hako ka nguruwe ili waweze kurejesha fedha zao.

Mama huo alikuwa amepewa nguruwe huyo mwenye umri wa miezi saba ili amlee, lakini baada ya maafisa wa mahakama kukuta hana kingine cha thamani zaidi ya nguruwe, wakaona bora wabebe mnyama huyo.

Mnyama huyo alichukuliwa baada ya mama huyo kusindwa kulipa deni hilo katika kipindi cha siku kumi alichopewa. Nguruwe mtoto kama huyo anaweza kuuzwa kwa zaidi ya dola mia tatu, katika jimbo la Primorye, ambalo mji wake mkuu ni Vladivostok. "Bado tunatafuta mteja" amesema mmoja wa maafisa waliomchukua nguruwe huyo.

Ombaomba matajiri

Katika visiwa vya Fiji, waziri wa kutokomeza umasikini v isiwani humo wamesema mitaa ya mji mkuu, Suva haina budi kusafishwa na omba omba wote kuondolewa, kwa sababu, hivi sasa wana uwezo wa kutosha wa kifedha. "Ombaomba sasa imekuwa fani yao, na sasa wana makazi mazuri na chakula" amesema waziri huyo akikaririwa na gazeti la Fiji Sun.

Waziri huyo ameongeza kuwa, baadhi yao wamejenga hadi nyumba ambazo wanapangisha watu wengine.

Amesema ombaomba wote hupatiwa dola hamsini hadi sitini kila mwezi. Waziri huyo,aitwaye Adi Ascenaca amesema zaidi ya hapo, hupata dola tisa au zaidi kila ziku kwa kuomba omba mitaani. Amesema ni mfano mbaya kwa watoto wanaokua, kwani wanaweza kuamua nao kuingia katika shughuli hiyo. Waziri huyo ametaka polisi kuwaondoa mitaani.

...na kwa taarifa yako

Na kwa taarifa yako.. Mtu mmoja kati ya watu bilioni mbili anaweza kufika umri wa miaka mia moja na kumi na sita , au zaidi.

Kisa na Mkasa haitakuwepo kwa wiki kadhaa, kupisha shughuli za uchaguzi wa Tanzania. Hakikisha unapiga kura..

Tukutane wakati mwingine....Panapo Majaaliwa.......

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali kutoka kwenye mtandao..