Mkuu wa waasi Rwanda akamatwa Ufaransa

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ilisema kiongozi wa kundi la FDLR la Rwanda alikamatwa nchini Ufaransa kwa makosa ya uhalifu wa kivita.

Katika hati ambayo ni siri, Callixte Mbarushimana anashutumiwa kwa makosa 11 ya mauaji, ubakaji na uhalifu mwengine uliofanywa wakati wa ghasia za muda mrefu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Image caption Callixte Mbarushimana

Mwaka jana aliiambia BBC kwamba alikana kuhusika na uhalifu wa kivita na wapiganaji wa FDLR hawakuwashambulia raia.

Wapiganaji wa FDLR hivi karibuni walishutumiwa kuwabaka mamia ya watu huko Congo.

Wakati huo huo, walio wengi Wahutu wa FDLR (Democratic Forces for the Liberation of Rwanda) walikana kuhusika na mashambulio katika mji wa Luvungi mashariki mwa Congo.

Baadhi ya viongozi wa FDLR wameshutumiwa kuhusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa kati Rwanda.

Baada ya kundi la Watutsi walio wengi kuidhibiti Rwanda, walikimbilia kwa ambapo kwa sasa kunajulikana kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kusababisha ghasia kwa miaka mingi eneo hilo.