Wamiliki Liverpool washindwa mahakamani

Klabu ya Liverpool imepiga hatua moja kukaribia kuuzwa kwa wamiliki wapya, huku kampuni ya New England Sports Ventures ikitumainiwa kushinda zabuni ya paundi milioni 300 iliyoafikiwa na bodi ya klabu.

Image caption Mashabiki wa Liverpool

Jaji Floyd akitoa uamuzi wake katika Mahakama Kuu alisema wamiliki wa sasa Tom Hicks na George Gillett hawana uwezo wa kuzuia uuzwaji wa klabu hiyo kwa wamiliki wa Boston Red Sox.

Mwenyekiti wa Liverpool Martin Broughton amesema bodi mpya ndio itaamua juu ya uuzwaji wa klabu hiyo.

Amesema: "Haitakuwa sahihi kuanza kufikiria kitakachoamuliwa na bodi."

Hicks na Gillett wametaka kuwepo ucheleweshwaji wa kusikilizwa maombi ya wanaoidai klabu hiyo benki ya Royal Bank of Scotland (RBS) kutoa amri isiyoweza kupingwa, ambayo itatoa nafasi kwa uwezekano wa kuuzwa wiki hii.

Lakini hata hivyo maombi hayo yalikataliwa na Jaji na kwa maombi ya benki ya RBS, mahakama imetoa amri kwa wamiliki hao wawili wakiwataka kufuata katiba iliyopo inayoongoza kanuni za makampuni na wakurugenzi waendeshaji.

Benki ya RBS sasa itaweza kupata fidia ya mkopo wake wa awali wa paundi milioni 237 unaowadai akina Hicks na Gillett.