Mgodi Chile: Miujiza yasherehekewa

Rais wa Chile amesema kamwe nchi yake haitarejea hali iliyokuwa nayo awali baada ya kukamilika kwa shughuli ya uokoaji wa wachimba migodi 33 waliokuwa wamenaswa chini ya ardhi kwa siku 69.

Image caption Rais wa Chile akiwa kwenye mgodi baada ya kazi ya uokoaji kukamilika.

Sebastian Pinera amesema anahisi wananchi wa Chile sasa "wana umoja zaidi na imara kuliko wakati mwingine wowote" na wanaothaminika kote duniani.

Kulikuwa na kila hali ya ushangiliaji wakati Luis Urzua, mwenye umri wa miaka 54, mchimbaji wa mwisho alipotolewa nje ya mgodi huo.

Shughuli hiyo iliyofanyika kwa saa 22, ilitekelezwa kwa kila mmoja wao kutolewa kwa kutumia chombo maalum. Wote sasa wamepelekwa hospitalini.

Baadhi yao wamebainika kuwa na matatizo ya meno, na wengine wanasumbuliwa na macho kutokana na kuishi katika vumbi na giza mgodini humo. Mmoja wao amegundulika kuwa na kichomi, ingawa hali yake inaelezewa kuwa si mbaya sana.

Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Jaime Manalich, alisisitiza kuwa wachimbaji wote wanaonekana kuwa katika afya njema kuliko ilivyokuwa ikitarajiwa. Haijawahi kutokea binadamu aliyenaswa chini ya ardhi kwa muda mrefu kiasi hicho kusalimika.

Wachimbaji hao walikuwa wamesalia na chakula cha kutosheleza kwa saa 48 wakati sehemu ya mgodi wa shaba na dhahabu wa San Jose nchini Chile katika jangwa la Atacama ulipoanguka tarehe 5 Agosti. Baada ya siku 17 za kuchimba kuwatafuta, hatimaye waokoaji walifanikiwa kuwasiliana nao.