Liverpool kwaendelea kuwaka moto

Wamiliki wa Liverpool wamesema mahakama moja ya Texas imetoa amri ya muda ya pingamizi dhidi ya kuuzwa kwa klabu hiyo.

Image caption Hali bado ni tete Liverpool

Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya rufaa ya wamiliki hao ambao ni Wamarekani, kutupwa na Mahakama Kuu kuhusiana na mchakato wa kuuzwa klabu hiyo.

Hicks na Gillett walitoa taarifa yao wakati bodi ya klabu ya Liverpool inakutana kuidhinisha kuuzwa kwa klabu hiyo kwa kampuni ya New England Sports Ventures.

Kwa kujibu hoja hiyo, bodi ya klabu imeahidi kutakuwa na uwezekano mkubwa amri hiyo ya mahakama ya Texas itaondolewa.

Taarifa ya klabu imeendelea kusema: "Kufuatia kumalizika vizuri kwa suala hilo katika Mahakama Kuu, bodi ya wakurugenzi ya Kop Football na Kop Holdings wakutane kumaliza kabisa suala la kuuzwa kwa klabu ya Liverpool kwa kampuni ya New England Sports Ventures.

"Kwa bahati mbaya, Thomas Hicks na George Gillett wamepata agizo la amri ya mahakama ya wilaya ya Texas dhidi ya wakurugenzi binafsi, Royal Bank of Scotland PLC na NESV, kuzuia uhamishaji wa pesa kukamilika.

Taarifa hiyo imeongeza kueleza:"Wakurugenzi binafsi wanaona amri hiyo ya mahakama si haki na inadhoofisha na hapana shaka itaondolewa ili kumaliza suala hilo kwa utulivu."

"Bodi ya klabu itaangalia upya suala hilo na itaomba ushauri wa kisheria. Hawawezi kupuuza pingamizi hili lililowekwa katika mahakama ya Texas licha ya kutokuwa na nguvu ya kimahakama nchini Uingereza.

Baada ya kupata pingamizi hilo la mahakama ya Dallas, Hicks na Gillett wamebainisha sasa wanadai zaidi ya paundi bilioni 1 za Uingereza kufidia hasara waliyopata.