Kiongozi mwingine afutwa kazi Niger

Bendera ya Niger
Image caption Bendera ya Niger

Mjumbe wa tatu katika uongozi wa kijeshi wa Niger amefutwa kazi.

Amri iliyosomwa kupitia televisheni ya kumfuta kazi Col Amadou Diallo kama waziri wa vifaa haikutoa sababu zozote ya hatua hiyo.

Mjumbe mwandamizi aliyeshikilia nafasi ya pili katika uongozi wa kijeshi, Colonel Abdoulaye Badie, na kiongozi wa majeshi ya taifa alilazimishwa kuachia ngazi mapema mwezi huu.

Kumekuwa na taarifa zinazopingana ikiwa Colonel Badie ametiwa mbaroni.

Hatua za kuwafuta kazi maafisa hao zinafanyika wakati kukiwa na uvumi kuhusu mzozo ulioibuka miongoni mwa viongozi wa kijeshi nchini humo, ambao walichukua madaraka katika mapinduzi yaliyofanyika mwezi February.

Kiongozi wa utawala huo wa kijeshi, General Salou Djibo, ameahidi kufanyika kwa uchaguzi mwezi January mwaka ujao.