FIFA yachunguza tuhuma za kuuza kura

Shirikisho la Kandanda Duniani FIFA limesema linachunguza madai kuwa wajumbe wake wawili wa kamati ya utendaji wanakusudia kuuza kura zao, katika kinyang'anyiro cha kuchagua nchi itakayoandaa Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022.

Image caption Kombe la Dunia

Gazeti la The Sunday Times la London limesema Amos Adamu kutoka Nigeria na Reynald Temarii wa Tahiti walijiandaa kujadiliana na waandishi wa habari waliojifanya wanaharakati wanaojaribu kuhakikisha Marekani inapewa nafasi ya kuandaa mashindano hayo.

Gazeti hilo linasema Bw Adamu alitaka kulipwa dola laki nane kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya nyasi bandia nchini Nigeria, wakati Bw Temarii alitaka malipo ya ujenzi ya kituo cha michezo.

Hiyo ni kwenda kinyume na kanuni za FIFA.

Picha za video zilizotolewa na gazeti la Sunday Times zimemuonesha Adamu akitaka fedha hizo alipwe yeye moja kwa moja kwa ajili ya kuidhinisha kinyang'anyiro hicho kwa Marekani.

Katika video hiyo, Adamu alihojiwa iwapo fedha hizo kwa "mradi binafsi" utakuwa na athari kuelekea upigaji wake wa kura.

Alijibu:"Bila shaka" itakuwa na athari. Hiyo haina shaka yoyote. Kwa sababu iwapo uwekeza utafanikiwa katika hilo, ina maana pia unahitaji kura.

Taarifa ya Fifa imesema: "Fifa na kamati yake ya maadili inafuatilia kwa karibu mchakato wa kinyang'anyiro cha kuwania kuandaa michuano ya Kombe la dunia kwa mwaka 2018 na 2022 na itaendelea kufanya hivyo.

Kwa vyovyote itakavyokuwa Fifa itachunguza suala hilo haraka na itaamua hatua za kuchukua bila kuchelewa.

"Wakati huo huo, Fifa imesema haipo katika nafasi kueleza zaidi juu ya tuhuma hizo."

Ila Shirikisho la Soka kwa nchi za Ocenic (OFC) limethibitisha linaifanyia kazi taarifa hiyo.

Katika taarifa yake OFC imesema inafahamu juu ya taarifa hiyo iliyotolewa na gazeti la Sunday Times la England. Na kwa maana hiyo inachunguza.

Kwa vyovyote vile safari hii ni zamu ya taifa la Ulaya kuandaa mashindano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2018 baada ya Marekani, taifa lisilo la Ulaya kujiondoa katika mbio hizo siku ya Ijumaa. Australia ilijiondoa mwezi wa Juni. Nchi zote hizo sasa zimeelekeza nguvu kwa ajili ya kuwania nafazi ya mwaka 2022.

Sasa England katika heka heka hizo itapambana na Urusi, Ubelgiji inayowania kwa pamoja na Uholanzi na Hispania inanyowania na Ureno.

Kura ya siri itapigwa tarehe 2 mwezi wa Desemba kuamua nani ataandaa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2018.