Sudan yapinga kikosi cha Umoja wa Mataifa

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa
Image caption Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa

Serikali ya Sudan imesema Umoja wa Mataifa hauwezi kupeleka wanajeshi wake wa kulinda amani kwenye maeneo yanayokumba na mizozo ya mpaka kati ya kusini na kaskazini.

Mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na kuweka amani, alitangaza kuwa askari wa usalama, watapelekwa katika maeneo ya mpakani yenye matatizo.

Mvutano unazidi nchini Sudan, wakati huu wa kukaribia kura ya maoni, ya mwezi Januari, kuamua kama eneo la Kusini linataka kujitenga.

Chama cha Rais Omar el Bashir, cha National Congress, kimesema kikosi chochote cha Umoja wa Mataifa kupelekwa katika eneo baina ya Sudan Kaskazini na Kusini lazima kiidhinishwe na serikali mjini Khartoum. Mkuu wa kuweka amani wa Umoja Mataifa, Alain Le Roy, alisema askari watapelekwa kwenye mpaka baina ya maeneo hayo. Hakueleza kama hao watakuwa askari zaidi, au ni wale-wale ambao tayari wako nchini Sudan.

Tangazo hilo lilitolewa, baada ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, ku-u-omba Umoja wa Mataifa, kulinda mpaka.

Lakini Sudan Kaskazini imekataa kata-kata wazo hilo. Maafisa wa daraja za juu wa chama cha NCP, pamoja na msaidizi wa rais katika usalama, Salah Gosh, wamesema Umoja wa Mataifa hauwezi kufanya hivo, bila ya idhini ya serikali.

Na mwanasiasa mashuhuri wa NCP, Ibrahim Ghandour, alisema, mvutano wowote unaweza kutatuliwa baina ya pande hizo mbili zenyewe.