Ethiopia: Fedha za misaada zatumiwa kununua wafuasi kisiasa

Image caption Raia wa Ethiopia wengi wanaishi katika hali ya umasikini na hutegemea misaada

Shirika la Human Rights Watch linadai kwamba serikali ya Ethiopia inawashinikiza raia wake kujiunga na chama tawala ili waweza kupata misaada. Wasipofanya hivyo wananyimwa usaidizi.

Shirika hilo linasema lilifanya uchunguzi wa miezi sita katika vijiji 53 nchini humo na kugundua kuwa kulikuwa na kampeni ya kuwanyima msaada raia waliojulikana kuwa wafuasi wa upinzani.

Na ili mfuasi huyo wa upinzani apate msaada anahitajika kuandika barua rasmi kuonyesha kuwa ameghairi na kujiondoa katika chama cha upinzani na kujiunga na chama tawala.

Serikali ya Ethiopia hutumia pesa za msaada kutoa misaada ya kilimo, elimu afya na huduma zingine muhimu kwa wananchi wake wengi wanaoishi katika hali ya umasikini.

Serikali ya Ethiopia imekuwa ikikanusha kabisa madai kama haya. Ethiopia ni moja ya nchi zinazopokea misaada mingi zaidi barani. Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka jana pekee, taifa hilo lilipokea takriban dola bilioni 3.

Shirika la Human Rights Watch linataka wanaotoa misaada kwa Ethiopia kufuatilia na kuhakikisha kuwa misaada hiyo inatolewa kwa raia bila ubaguzi.