Misri yaporomoka ngazi moja ya Fifa

Mabingwa wa soka barani Afrika Misri, wameporomoka katika nchi kumi bora za soka duniani kutokana na viwango vipya vilivyotolewa na Fifa siku ya Jumatano.

Image caption Sasa inashika nafasi ya 11 kwa ubora duniani

Mafarao hao waliokuwa wakishikilia nafasi ya kumi sasa wameshuka kidogo hadi nafasi ya 11 duniani, kwa maana hiyo hakuna nchi ya Afrika iliyo miongoni mwa timu kumi bora duniani.

Ghana imesogea nafasi tatu juu hadi ya 17, wakati Ivory Coast imechupa nafasi nne juu na inashikilia nafasi ya 19.

Mabingwa wa soka duniani na bara Ulaya Hispania, bado wameendelea kushikilia usukani wa nchi bora kwa kutandaza soka duniani, wakati Uholanzi iliyocheza nayo fainali ya Kombe la Dunia, ipo nafasi ya pili na Brazil imesogea hadi nafasi ya tatu.

Wakati huo huo, Tunisia nayo imepanda hadi nafasi ya nafasi 11 juu na kuingia katika timu kumi bora za Afrika.

Nchi iliyofanikiwa kupanda viwango cha ubora wa soka Afrika ni Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambayo imeruka nafasi 60 na sasa inakamata nafasi ya 112 katika viwango vya ubora duniani hasa baada ya kuilaza Algeria mabao 2-0 mapema mwezi huu kutafuta timu zitakazofuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika.

Hayo ni mafanikio makubwa kwa nchi hiyo ya Afrika ya Kati kupanda kwa kiwango cha soka.

Niger, ambayo pia ilipata ushindi wa kushangaza ilipoilaza Misri bao 1-0, nayo imepanda nafasi 54 na sasa kwa ubora barani Afrika inakamata nafasi ya 26 na kwa dunia ni ya 100.

Viwango vipya vya ubora wa soka Afrika na ubora wa dunia kwenye mabano

1. Misri (11)

2. Ghana (17)

3. Ivory Coast (19)

4. Algeria (33)

5. Nigeria (34)

6. Burkina Faso (37)

7. Cameroon (38)

8. Gabon (39)

9. Tunisia (45)

10. Guinea (47)