Ferguson asema Rooney anataka kuondoka

Sir Alex Ferguson
Image caption Sir Alex Ferguson

Sir Alex Ferguson amebainisha mshambuliaji Wayne Rooney anataka kuondoka Manchester United.

Meneja huyo wa klabu hiyo ya Old Trafford amekiri "alishtushwa" na "kukatishwa tamaa" kusikia habari hizo, lakini amesema bado anapenda kuchezea timu ya taifa ya England.

"Tumeshangazwa kama wengine, hatuelewi kwa nini anataka kuondoka," alisisitiza Ferguson.

Ferguson amesema "mlango uko wazi" kwa Rooney, kubakia katika klabu hiyo aliyojiunga mwaka 2004 akitokea Everton.

Mkataba wa Rooney na klabu hiyo kubwa ya Ligi Kuu ya England, unamalizika mwishoni mwa msimu wa mwaka 2011/12.

Manchester United itacheza na Bursaspor katika ligi ya mabingwa wa Ulaya siku ya Jumatano, lakini Rooney hatacheza baada ya kutolewa nje ya uwanja kwa machela wakati wa mazoezi siku ya Jumanne.

Mustakabali wa Rooney limekuwa suala lililokuwa na utata mkubwa kwa siku chache zilizopita, baada ya taarifa kuwa mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya England hakuwa tayari kuingia mkataba mpya.

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha klabu hiyo MUTV kabla hajazungumza na vyombo vingine vya habari, Ferguson amesema Mkurugenzi Mkuu wa Manchester United David Gill amemueleza kuhusu uamuzi wa Rooney wa kukataa kuingia mkataba mpya.

"Ilikuwa tarehe 14 mwezi wa Agosti ambapo David alinipigia simu kunifahamisha Rooney hatasaini mkataba mpya," alisema Ferguson.

"Nilishangazwa. Maana ni miezi michache tu alitamka yupo katika moja ya vilabu vikubwa duniani.

"Niliomba kukutana nae, akakiri kupitia wakala wake akasema anataka kuondoka."