Kiongozi wa Upinzani Rwanda Mahakamani

Image caption Ingabire amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za uhaini

Kiongozi wa Chama cha upinzani nchini Rwanda, FDU Inkingi, Ingabire Victoire amefikishwa mbele ya mahakama na kusomewa mashtaka mapya ya uhaini.

Ingabire alikamatwa wiki iliyopita kwa tuhuma za uhaini na kushirikiana na makundi ya kigaidi kuhujumu usalama wa Rwanda.

Upande wa mashtaka umeelezea kwamba Bi Ingabire alikamatwa baada ya madai yaliyotolewa na mwanajeshi wa zamani Meja Vital Uwumuremyi, aliyekamatwa mnamo Jumatano wiki iliyopita.

Mwanajeshi huyo wa zamani anadaiwa kuwapa maafisa wa upelelezi fununu kwamba alipata msaada kutoka kwa mwanasiasa huyo kubuni kikundi cha kijeshi cha chama hicho cha FDU.

Madai haya yamekanushwa na vyama vya upinzani nchini humo.

Mwanasiasa huyo alirejea nchini Rwanda kutoka ushamishoni kwa lengo la kugombea kiti cha urais katika uchaguzi uliofanyika Agosti mwaka huu.

Watetezi wa haki za binadamu wanailaumu serikali ya Rwanda kwa kuwakandamiza wapinzani.

Hata hivyo Rais Paul Kagame amekuwa akikanusha madai haya kwa kusema kuwa serikali yake inatawala kwa misingi ya haki na haitaruhusu mtu yeyote kuvuruga amani.