Bei za tikiti za Olympic London zatolewa

Tikiti kwa ajili ya michezo ya Olympic ya mwaka 2012 itakayofanyika London zimetolewa, huku kuona fainali ya mbio za mita 100 gharama yake ni paundi za Uingereza 725.

Image caption Uwanja wa Olympic London

Waandaaji wa mashindano hayo ya London 2012 pia wamebainisha tikiti kwa ajili ya sherehe za ufunguzi zitauzwa kati ya paundi 20.12 na 2,012.

Kwa tikiti milioni 8.8 zinazopatikana, asilimia 75 zitauzwa hadharani kuanzia mwezi Machi mwaka 2011.

Na tikiti 125,000 zimewekwa maalum kwa ajili ya wanafunzi wa shule ambao watawajibika kufaulu jambo fulani ili waweze kupata tikiti hizo.

Waandaaji wa michezo hiyo ya London 2012 wamesema asilimia 90 ya tikiti zitauzwa kati ya paundi 100 au chini ya hapo, asilimia 66 zitauzwa chini ya paundi 50 na nyingine kiasi cha asilimia 25 zitamgharimu mtazamaji paundi 20 au chini ya hapo.

Bei za tikiti kwa ajili ya kuangalia fainali za mbio za mita 100 kwa wanaume zitakuwa kati ya paundi 50 hadi 725, wakati zile za kuangalia fainali za mbizo za mita 100 kwa wanawake bei ni kati ya paundi 50 hadi 450.

Michezo mingine muhimu, kama fainali za mbio za baiskeli tikiti zitakuwa kati ya paundi 50 hadi 325 na michezo ya fainali za kuchupa majini gharama yake itakuwa kati ya paundi 50 na 450.

Sehemu ya michezo mingine kama mbio za nyika ama marathon , mbio za baiskeli za barabarani na triathlon itakuwa bure.

Kuanzia mwezi Machi, watu wanaweza kujisajili wanapendelea kuangalia michezo gani na iwapo watajitokeza watu wengi zaidi, basi tikiti zitauzwa kwa mtindo wa kupiga kura.

Hadi sasa watu milioni 1.7 wamekwishajisajili kuangalia mashindano ya London 2012.