AU: Vikwazo viwekewe Somalia

Image caption Majeshi ya AU yamekuwa yakikabiliana na wanamgambo nchini Somalia

Muungano wa Afrika umeitisha vikwazo vya usafiri wa anga na maji kuwekewa Somalia katika juhudi za kukabiliana na uharamia na wanamgambo wa kiislam nchini humo.

Kamishna wa masuala ya amani na usalama katika muungano huo Ramtane Lamamra ameambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa vikwazo hivyo vitasaidia kuzuia silaha kuingia nchini humo na kuthibiti usafiri wa wapiganaji.

Lamamra ameelezea kuwa Muungano huo unahofu kwamba maasi ambayo yanaendela nchini humo tayari yameanza kuenea katika mataifa jirani.

Bw Lamamra ameshutumu sera ya Umoja wa Mataifa kuhusu Somalia akisema kuwa mipango mingi kuhusu nchi hiyo inatekelezwa shingo upande.

Ametaka idadi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Muungano huo kuongezwa kutoka elfu nane hadi elfu ishirini.

Somalia haijakuwa na serikali dhabiti kwa zaidi ya miaka ishirini na kwa hivi sasa serikali ya muda inakabiliana na wapiganaji wa kiislam ambao wanaendeleza mapigano kote nchini humo.