Ripoti ya mtaalamu wa silaha Uingereza yachapishwa

 Dk David Kelly
Image caption Aliyekuwa mtaalamu wa silaha

Serikali ya Uingereza imechapisha ripoti za siri kuhusu kifo cha mtaalam wa maswala ya silaha nchini humo Dk David Kelly miaka saba iliyopita.

Dr Kelly alipatikana ameuwawa baada ya kufichuliwa kwamba yeye ndiye alikuwa chanzo cha ripoti iliyotangazwa na BBC ambayo iliishutumu serikali ya Uingereza kwa kutia chumvi sababu za kuivamia Iraq chini ya utawala wa Saddam Hussein.

Baadhi ya watu wametilia shaka matokeo ya uchunguzi uliobaini kuwa alijiuawa.

Hata hivyo stakabadhi zilizotolewa hivi leo zinaonyesha kuwa vidonda vilivyokuwa katika mwili wa Dk Kelly vinaonyesha kuwa huenda alijidhuru mwenyewe.

Kufichuliwa kwa taarifa hizo na kifo cha Dk Kelly kulizua uhasama mkubwa kati ya BBC na serikali ya Uingereza na kusababisha kujiuzulu kwa mwenyekiti na mkurugenzi mkuu wa BBC.