Wikileaks yafichua siri za jeshi la Marekani

Wanajeshi wa Marekani nchini Iraq
Image caption Wanajeshi wa Marekani nchini Iraq

Maelfu ya nyaraka mpya za siri za Marekani zilizovuja zinaeleza kuwa makamanda wa Marekani walijua kuwa askari wa Iraqi walikuwa wakiwatendea vibaya wafungwa, lakini wakashindwa kuchukua hatua.

Nyaraka hizo zilizochapishwa na tovuti ya Wikileaks zinaelezea mateso, unyanyasaji and mauaji ya wafungwa wa Iraq waliotiwa mbaroni na majeshi ya Iraq katika miaka ya 2004 na 2009.

Baadhi ya nyaraka hizo zinaonyesha kuwa kati kesi nyingi wanajeshi wa Marekani walitoa ripoti kuhusu udhalishishaji huo, lakini wakaamrishwa kutofanya uchunguzi.

Katika tukio moja, zinaeleza ndege ya helicopter ya Marekani ikipatiwa ruhusa ya kuwarushia mabomu kundi la waasi wa Iraq waliokuwa wakijaribu kujisalimisha.

Marubani wa ndege hiyo waliambiwa kuwa waasi hao hawawezi kujisalimisha kwa ndege na inakubalika kuwashambulia.

Pia kuna taarifa za serikali ya Iran kujihusisha na masuala ya Iraq, huku kukiwa na waasi wanaotumia silaha zilizotolewa na jeshi maalum la Iran lijulikanalo kama Iranian Republican Guard.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ,Hillary Clinton, alilaani ufichuzi wa habari zozote za siri ambazo zinahatarisha usalama wa taifa au kuhatarisha maisha ya wanajeshi wa kimataifa au raia.

Mwandishi wa BBC wa masuala ya ulinzi anasema nyaraka hizo zimechujwa kwa hali ya juu ili kuondoa taarifa ambazo zinaweza kuwatambua baadhi ya watu.