Arsenal yainyoa Manchester City 3-0

Mabao ya Samir Nasri, Alex Song na Nicklas Bendtner yameiwezesha Arsenal kuwafunga mahasimu wao wakubwa Manchester City .

Image caption Wachezaji wa Arsenal wakipongezana

City ilianza vibaya mchezo huo baada ya mlinzi wao wa kutegemewa Dedryk Boyata kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Marouane Chamakh huku akiwa mchezaji wa mwisho nyuma.

Pamoja na ushindi huo nahodha wa Arsenal Cesc Fabregas alikosa mkwaju wa penalti uliodakwa na mlinda mlango Joe Hart wa Manchester City.

Kwa kiasi kikubwa Arsenal waliumiliki mchezo huo kwa pasi zao murua.

Matokeo hayo yanaifanya Arsenal kuwa nafasi ya pili ikiwa na pointi 17, nyuma ya Chelsea inayoongoza kwa pointi 22.

Katika mchezo wa awali mabao mawili yaliyowekwa kimiani na Javier Hernandez yameiwezesha Manchester United kuzoa pointi tatu muhimu dhidi ya Stoke City.

Manchester United nayo sasa imefikisha pointi 17 ikishikilia nafasi ya tatu. Mnacheseter United walishinda kwa mabao 2-1.

Nayo Liverpool ilizinduka kutoka usingizini ilipoichapa Blackburn mabao 2-1. Huo ni ushindi wa kwanza wa Liverpool tangu mwezi wa Agosti katika uwanja wao wa Anfield. Hata hivyo pamoja na kupata pointi tatu, bado Liverpool ipo nafasi ya 18.

Mabao ya Liverpool yalipachikwa na Sotirios Kyrgiakos katika dakika ya 48 kwa kichwa cha nguvu alipounganisha kona ya Steven Gerrard.

Blacburn walipata bao lao baada ya mlinzi Carragher kujifunga mwenyewe katika dakika ya 50. Dakika tatu baadae Ferdinando Torres akaipatia bao la ushindi Liverpool lililoipa pointi tatu muhimu.

Kwa matokeo hayo Liverpool sasa imezoa pointi 9.