Platini apinga teknolojia ya golini

Rais wa Uefa Michel Platini amezidi kupinga matumizi ya teknolojia golini, akidai itaufanya mchezo wa soka sawa na "kitu cha kuchezea" na hautakuwa halisi.

Image caption Michel Platini

Fifa imefungua upya mjadala wa suala hilo, lakini Platini amesema suluhisho la utata unaojitokeza iwapo bao limeingia au la, ni kuweka mwamuzi msaidizi nyuma ya lango na waamuzi waheshimiwe.

"Waamuzi hawana budi kusaidiwa na vilabu, mashabiki, vyombo vya habari na mamlaka zinazohusika," alieleza hayo kupitia mtandao wa Chama cha Soka cha Scotland.

Akasema ndio maana wao wameamua kuongeza waamuzi wasaidizi wawili nyuma ya lango katika michezo ya ubingwa wa Ulaya.

Wiki iliyopita, Bodi ya Shirikisho la Soka Duniani (IFAB), chombo chenye kutoa uamuzi mbalimbali kwa Fifa, ilizitaka kampuni za teknolojia kuwasilisha mawazo yao kuhusiana na suala hilo itakapofika mwishoni mwa mwezi wa Novemba.

Utaratibu huo baadae utajaribiwa kabla ya mkutano ujao wa IFAB utakaofanyika mwezi wa Machi, ambapo utaratibu wa utekelezaji wa mpango huo utajadiliwa kwa kina.

Lakini Platini amesema kuongeza macho mengine ya ziada nyuma ya lango, ndio inavyotokea katika michezo ya Ubingwa wa Ulaya na ni suluhisho lenye mantiki.

"Mwamuzi mmoja hatoshi, hasa katika enzi hizi zenye kamera 20 uwanjani" Alieleza zaidi Platini, ambaye alianza kushika hatamu za kuongoza Uefa tangu mwaka 2006.

Aliongeza:"Haitakuwa haki wakati kamera zinaona kila kitu, lakini mwamuzi ana macho mawili hawezi kuona kila kitu. Kila mara anafanya makosa na kamera zipo kuangalia hayo makosa.

Fifa iliondoa majaribio ya kutumia teknolojia ya kubaini bao limeingia au la mwaka 2008, baada ya kuamua utaratibu huo unaotumika katika michezo mingine kama tennis na kriketi haufai kwa mchezo wa soka.

Fifa pia ilijaribu utaratibu huo kwa kuweka kifaa maalum ndani ya mpira, lakini ikaona inatatanisha mno na pia haitoi jawabu sahihi.

Lakini baada ya matukio ya hivi karibuni, ikiwemo bao la Frank Lampard katika Kombe la Dunia lililokataliwa England ilipocheza na Ujerumani na kufungwa mabao 4-1 mwezi wa Juni, licha ya kuonekana wazi mpira ulikuwa umevuka mstari langoni, Fifa iliamua kuliangalia suala hilo na kutafuta uwezekano wa kulipatia ufumbuzi.

Rais wa Fifa Sepp Blatter amesema haitakuwa jambo la busara kutolijadili upya suala hilo la teknolojia na amelipeleka suala hilo kwa bodi ya IFAB.