Kombe la Dunia 2018 England yalalamika

Jopo la England linalosimamia kinyang'angiro cha kuwania Kombe la dunia mwaka 2018 limepeleka malalamiko mbele ya Fifa dhidi ya matamshi ya kiongozi wa kikosi cha Urusi kinachopiga kampeni ya kuwania kuandaa Kombe hilo la Dunia kuhusu London.

Image caption England yailalamikia Urusi

Kiongozi huyo wa kikosi cha Urusi kwa kuwania nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia mwaka 2018 Andrei Sorokin alinukuliwa akisema London ni jiji lenye uhalifu wa kupindukia na vijana wadogo wanaokunywa pombe sana.

Fifa inakataza kabisa kushutumiana baina ya nchi zinazowania kuandaa mashindano yake.

Sorokin amesema hakuwa na nia ya kudhoofisha uwezo wa England katika kuandaa mashindano hayo na yupo tayari kuomba msamaha kwa lolote ambalo "hakueleweka vizuri".

Alisema:"Nipo tayari kuomba msamaha kutokana na kutoeleweka vizuri. "Tunao mkanda wa mahojiano na nafahamu sijavunja kanuni yoyote.

Malalamiko ya England yameelekezwa zaidi kwa Sorokin na sio kwa Urusi.