Uwanja wa Nyayo Kenya wafungwa

Maafisa wa serikali ya Kenya wamefunga kwa muda usiojulikana viwanja viwili vya michezo mjini Nairobi kufuatia vifo vya mashabiki wa soka wanane baada ya kutokea mkanyagano.

Image caption Uwanja wa Nyayo

Viwanja vilivyofungwa ni Nyayo na City.

Kwa mujibu wa mwenyekiti Kampuni ya Soka ya Kenya, Mohammed Hatmy: "Kufungia viwanja hivyo kwa michezo yote ya soka ni uamuzi mzuri."

Wakati huohuo, Rais wa Fifa Sepp Blatter ametuma salamu za rambirambi kwa wapenzi wa soka wa Kenya baada ya mkasa wa siku ya Jumamosi.

Polisi nchini Kenya wamo katika uchunguzi kubaini kilichosababisha mkasa ule, uliotokea katika mechi ya ligi baina ya timu maarufu za Gor Mahia na AFC Leopards, licha ya kwamba uwanja ulikuwa haujajaa sana.

Waziri Mkuu Raila Odinga ameonesha matumaini yake uchunguzi utakamilika itakapofika mwishoni mwa wiki hii.

Mwaka 2005 tukio kama hilo la kukanyagana lilitokea katika uwanja wa Nyayo, ambapo kijana mmoja alikufa baada ya kukanyagwa wakati wa mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia kati ya Harambee Stars na timu ya taifa ya Morocco.

Matokeo yake, Fifa ilipiga marufuku kutumika kwa uwanja huo kwa muda wa miezi sita wakati serikali ya Kenya iliahidi kufanya uchunguzi na hadi sasa hakuna kubwa lililofanyika.

Uchunguzi wa hivi sasa unalenga kubaini juu ya uuzaji wa tikiti na ulinzi kwa mechi za ligi.

Mashabiki sita waliuawa siku ya Jumamosi katika uwanja wa Nyayo na wengine wawili wakapoteza maisha hospitalini kutokana na majeraha waliyopata.

KFL imesema uwanja wa City umeingia mkumboni kufungiwa kwa sababu utawala wa uwanja huo umeshindwa kutekeleza maelekezo ya kufikia viwango vya Fifa.