Hodgson aionya Man United kwa Pepe Reina

Meneja wa Liverpool Roy Hodgson ameionya Manchester United kwamba mlinda mlango Pepe Reina hauzwi.

Image caption Pepe Reina

Meneja wa Man United Sir Alex Ferguson amekuwa akihusishwa kumnyemelea mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 28, wakati siku za nyuma Arsenal nayo ilisemwa ilikuwa ikimuhitaji Reina.

Hodgson amesema:"Iwapo Ferguson anamzengea Reina kwa kuwa anazo fedha, basi atakuwa anamtaka mlinda mlango huyo kwa vile ni hodari".

"Lakini hatutaki kumuuza. Yeye ni sawa na damu yenye kuleta uhai ndani ya timu yetu", ameongeza Hodgson.

Reina alijiunga na Liverpool akitokea klabu ya Villarreal kwa kitita cha paundi milioni 6 mwezi Julai mwaka 2005 na amekwishaicheza mechi 271 katika klabu hiyo.

Ameingia mkataba mpya wa miaka sita mwezi wa Aprili, lakini baada ya Liverpool kushindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na kutimuliwa kwa meneja Rafael Benitez, mlinda mlango huyo alihusishwa kujiunga na Arsenal kwa kitita cha paundi milioni 23.

Kwa wakati huu kuna uwezekano wa mshambuliaji Fernando Torres na Pepe Reina wakaupiga chenga mkataba wao na huenda wakaondoka wakati wa usajili mdogo mwezi wa Januari

Reina amebakia Liverpool wakati wa mwanzo mbaya wa msimu huu na mzozo wa wamiliki ulipomalizika na sasa kumilikiwa na kampuni ya New England Sports Ventures, bado uvumi wa kuondoka ungalipo.

Taarifa za hivi karibuni zinamhusisha Reina kujiunga na Manchester United, ambapo anatazamiwa kuchukua nafasi ya Edwin van der Sar mwenye umri wa miaka 39.

Lakini Hodgson amesisitiza klabu ya Liverpool haina nia ya kumuuza mlinda mlango huyo na akaongeza, hadi sasa hawajasikia lolote kutoka Manchester United na zaidi ya hapo hawataki kusikia chochote kutoka Manchester United.