Fifa yang'ang'ania tarehe Kombe la Dunia

Rais wa Fifa Sepp Blatter amesema tarehe ya kura kuamua nchi gani zitaandaa Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022 itabakia kuwa ile ile tarehe 2 Desemba.

Image caption Sepp Blatter

Fifa imetoa uamuzi huo licha ya wajumbe wake wawili wa kamati ya utendaji kusimamishwa kwa tuhuma za kuuza pesa.

Blatter amesema:"Tumesaliwa na wiki tano kabla hatujatoa uamuzi wa mwisho, kwa hiyo hakuna sababu ya kubadilisha chochote".

"Kwa hiyo tarehe 2 Desemba kamati ya utendaji itatoa uamuzi kwa kupiga kura ya siri nchi zipi ziandae Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022."

Licha ya Fifa kuamua kuendelea na tarehe hiyo, Blatter amekiri huenda itakuwa ni makosa kuendesha mchakato wa kura ya kutafuta nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia kwa mashindano mawili kwa wakati mmoja.

Heshima ya Fifa itaendelea kubakia pale pale. Wale wote walio ndani na nje ya Fifa wanafahamu hilo Wajumbe wawili wa kamati ya utendaji ya Fifa waliosimamishwa ni Amos Adamu kutoka Nigeria na Reynald Temarii kutoka Tahiti, na kwa sasa wanachunguzwa na jopo la Fifa linalosimamia maadili.

Blatter amethibitisha uamuzi kuhusu hatma yao utatolewa tarehe 17 mwezi wa Novemba na iwapo hawatarejeshwa kwenye uongozi, basi wajumbe 22 tu waliosalia wa kamati ya utendaji ya Fifa watapiga kura badala ya wajumbe kamili 24.