Chelsea yajikita kileleni yailaza Rovers

Chelsea imezidi kujisogeza mbele kuelekea kutetea taji lake la Ligi Kuu ya soka ya England, baada ya kuwalaza Blackburn Rovers mbele ya uwanja wao wa Ewood Park.

Image caption Chelsea yashinda

Walikuwa ni Blackburn walioanza kupata bao lililofungwa na Benjani Mwaruwari kwa kichwa dakika ya 21.

Chelsea walijifunga kibwebwe na kufanikiwa kusawazisha kwa bao la Nicolas Anelka katika dakika ya 39.

Baada ya hapo ilikuwa ikielekea kama timu hizo zingetoka sare, lakini dakika ya 83 alikuwa Branislav Ivanovic akaweka hai matumaini ya Chelsea kutetea taji lake, kwa kufunga ba zuri la kichwa baada ya pasi ya Yuri Zhirkov.

Kwa ushindi huo Chelsea imejikita kileleni kwa kuzoa pointi 25.

Nayo Arsenal ikicheza nyumbani katika uwanja wa Emirates, walibanwa vilivyo na West Ham timu iliyo mkiani hadi ziliposalia dakika mbili kabla mpira kumalizika, ndipo Alex Song akapachika bao zuri la kichwa na kuendelea kushikilia nafasi ya pili ikiwa na pointi 20.

Katika mchezo huo Arsenal waliumiliki kwa kiasi kikubwa na kupoteza nafasi nyingi za kufunga mapema, kutokana na ustadi wa mlinda mlango wa West Ham, Robert Green aliyefanya kazi kubwa kuinyima kuokoa mabao ya wazi kutoka wachezaji wa Arsenal waliokuwa na uchu wa kufunga.

Bao la Arsenal lilianzia kwa mkwaju wa Samir Nasir uliogonga mwamba na Wolcott akaurudisha tena ndipo ukamkuta Song aliyeujaza kwa kichwa wavuni.

Katika mchezo mwengine Everton waliilaza Everton baada ya Yakubu kufunga bao lake la kwanza msimu huu na kuifanya klabu hiyo kutofungwa katika michezo mitano mfululizo ya ligi hadi sasa.

Matokeo hayo yanaipeleka Everton hadi nafasi ya saba wakiwa na pointi 13.

Mabao mawili yaliyofungwa kipindi cha kwanza na Clint Dempsey yaliiwezesha Fulham kuwalaza Wigan kwa mabao 2-0.

Fulham sasa wamesogea nafasi ya nane na pointi zao 12.

Hali bado inaonekana si shwari kwa Manchester City, klabu iliyotumia pesa nyingi kusajili wachezaji nyota duniani baada ya kulazwa na Wolves mabao 2-1.

Wiki iliyopita Manchester City waliadhiriwa nyumabi kwao na Arsenal kwa kufungwa mabao 3-0.

Walikuwa ni Man City walioanza kuufungua mlango wa Wolves kwa bao la mkwaju wa penalti alilofunga Emannuel Adobayor dakika ya 23.

Nenad Milijas alisawazisha bao hilo katika dakika ya 30. Na alikuwa David Edwards aliyeshindilia msumari wa mwisho kwa Man City alipofunga bao la pili na kuonekana ni ushindi wa kushangaza. Pamoja na ushindi huo Wolves wameendelea kushikilia nafasi ya pili kutoka mkiani lakini sasa wamejizolea pointi 9 wakiiacha West Ham yenye pointi 6 mkiani.