Rooney kutocheza wiki tano

Mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney hataweza kucheza kwa wiki tano zijazo, kwa mujibu wa Sir Alex Ferguson.

Image caption Wayne Rooney

Rooney aliyesaini hivi karibuni mkataba wa mpya utakaomuweka Old Trafford kwa miaka mitano, kwa sasa anatibu kifundo cha mguu alichoumia mazoezini tarehe 19 mwezi wa Oktoba.

Meneja wa Man United Ferguson alisema:"Natumai Wayne atakuwa nje kwa wiki nyingine tano."

"Anatakiwa kurejesha ule uimara wake wa mchezo. Nadhani wiki tano zitatosha."

Rooney awali alitazamiwa kukaa nje ya uwanja kwa wiki tatu, na kuweka matumaini ya kuweza kucheza mechi na mahasimu wao wakubwa Manchester City tarehe 10 Novemba. Lakini Ferguson ametupilia mbali uwezekano huo na kuongeza: "Hana nafasi hiyo. Mchezaji yeyote anayekuwa nje ya uwanja kwa wiki chache, unahitaji awe imara kwa asilimia 100 na si chini ya hapo."

Rooney, ambaye alikuwa mapumzikoni Dubai pamoja na mkewe, amekosa kuichezea Man United michezo minne iliyopita, ikiwemo mechi ya Jumamosi walipoifunga Tottenham mabao 2-0 ambapo alikuwa mtazamaji.

Mechi yake ya mwisho kuichezea Manchester United ilikuwa ni dhidi ya West Brom tarehe 16 Oktoba timu hizo zilipotoka sare ya mabao 2-2.

Iwapo atakuwa nje kwa wiki tano zijazo, atakosa mechi dhidi ya Bursaspor, Wolves, City, Aston Villa, Wigan, Rangers, Blackburn na Blackpool.