Upigaji kura wamalizika Tanzania

Mamilioni ya Watanzania wamejitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, uchaguzi ambao kwa jumla umekwenda kwa hali ya utulivu licha ya matatizo na vurugu za hapa na pale.

Image caption Slaa na Kikwete

Wapiga kura kadha hawakuweza kupiga kura kutokana na majina yao kutokuwemo katika daftari la wapigaji kura, kwingineko karatasi za kupigia kura zilichelewa kufika au hazikufika kabisa.

Katika visiwa vya Zanzibar, karatasi za kupigia kura katika uchaguzi wa rais na wabunge wa muungano zilikosekana katika vituo mbalimbali.

Uchaguzi wa madiwani umelazimika kuahirishwa hadi siku zijazo kwa sababu hizo hizo.

Vituo vya uchaguzi vimefungwa rasmi saa kumi jioni, huku kazi ya kuhesabu kura ikianza katika vituo hivyo.

Wapiga kura milioni 19.6 walitarajiwa kushiriki katika upigaji wa kura.

Wakati huo huo Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania imetangaza imeahirisha Uchaguzi katika baadhi ya Majimbo na Kata kutokana na upungufu uliojitokeza hususan katika karatasi za kura.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Rajabu Kiravu, Kata na Majimbo ambayo uchaguzi wake umeahirishwa ni kama ifuatavyo:-

1. Uchaguzi wa Wabunge katika majimbo ya Nkenge, Mpanda Mjini na Mpanda vijijini. Kwa upande wa Zanzibar (Unguja) Majimbo ya Mwanakwerekwe, Mtoni na Magogoni, na Wete (Pemba)

2. Uchaguzi wa Madiwani katika kata zifuatazo:- Na. HALMASHAURI KATA 1. Newala DC Mtonya

2. Mbulu DC Endegikot

Hata hivyo katika majimbo hayo matatu ambapo Uchaguzi wa Wabunge umeahirishwa, uchaguzi wa Rais na Madiwani umefanyika kama ilivyopangwa.

Vile vile, katika Kata ambazo Uchaguzi wa Madiwani umeahirishwa, Uchaguzi wa Rais na Wabunge umefanyika kama ilivyopangwa.

Tume hiyo ya Taifa ya Uchaguzi imesema tarehe za kufanyika uchaguzi huo itatangazwa hapo baadaye.