Man City hakuna mkwaruzano na kocha wao

Kiungo Gareth Barry amesisitiza wachezaji wa Manchester City wanamuunga mkono bosi wao Roberto Mancini.

Image caption Roberto Mancini

Mancini alikwaruzana na mshambuliaji Carlos Tevez na pia mchezaji wa zamani wa timu hiyo Craig Bellamy, wakati kulikuwa na taarifa za kutoelewana miongoni mwa wachezaji wa klabu hiyo.

Kwa mujibu wa Barry: "Ukweli kuna kundi la wachezaji wanaoshirikiana, wakifanya kazi kwa bidii na kufanya kazi kwa ajili ya bosi."

Kiungo huyo wa timu ya England pia ameomba msamaha kwa meneja Mancini baada ya kuonekana kwenye kamera anakunywa pombe huko Scotland alipokuwa mapumziko.

Alisema: "Nasikitika hilo limetokea kwa upumbavu wangu. Kamwe hilo halitatokea tena, aliongeza Barry ambaye alikuwa pamoja na wachezaji wenzake Joe Hart na Adam Johnson katika karamu hiyo ya Scotland.

"Nilimuomba radhi meneja, tulikwenda kinyume lakini hayo yamepita na sasa tunaganga yajayo", alisema Barry. Akaongeza: "Kila mtu katika chumba cha kubadilishia nguo na mazoezini anataka kuifanyia vizuri Manchester City."

Kauli ya Barry ya kuomba radhi na taarifa ya umoja uliopo katika chumba cha kubadilishia nguo imetolewa baada ya Manchester City kufungwa mfululizo katika mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu ya England, na hali haikuwa shwari kwa meneja Mancini.

Man City walifungwa mabao 3-0 na Arsenal na wiki moja baadae wakalazwa na Wolves mabao 2-1.

Nae mlinzi wa timu hiyo Kolo Toure amesema; Wachezaji tunapaswa kuchukua jukumu kubwa zaidi".

Aliongeza: "Unapochezea moja ya vilabu tajiri duniani, unahitajika kujituma uwanjani."

Man City wameshinda mechi tano tu kati ya mechi 10 za ligi kuu ya England na kwa sasa wameachwa kwa pointi nane na vinara wa ligi hiyo Chelsea.

Klabu hiyo imetumia pesa nyingi sana msimu huu kusajili wachezaji wenye majina makubwa akiwemo James Milner na mshambuliaji Mario Balotelli, kwa hiyo kufungwa hivi karibuni kumeleta hisia mbaya ndani ya timu hiyo, huku baadhi ya magazeti yakiandika mzozo miongoni mwa wachezaji na baadhi ya wachezaji wakiwa hawafurahishwi na mbinu za ufundishaji wa Mancini.

Mshambuliaji Emmanuel Adebayor na mlinzi Vincent Kompany walionekana wakitoleana maneno siku ya Jumamosi walipofungwa na Wolves, wakati Yaya Toure na Milner walizozana wakati wa mapumziko katika mechi waliyopewa kipigo na Arsenal.

Toure aliondoka uwanjani kabla mchezo kumalizika baada ya kutolewa wakati wa mapumziko, huku afisa mmoja wa klabu hiyo akieleza lilikuwa ni "jambo la kawaida" ili aweze kuwahi nyumbani kutokana na hali ya "foleni barabarani".

Kaka yeke Kolo Toure amesema wachezaji wanakubali kulaumiwa, lakini akasisitiza hakuna mzozo miongoni mwao.