Dr. Shein ndiye rais wa Zanzibar

Dr. Ali Mohammed Shein ameapishwa rasmi leo asubuhi kuwa rais wa kisiwa cha Zanzibar.Shein aliapishwa katika uwanja wa Amaan.

Maelfu ya watu walianza safari yao mapema asubuhi ili kuhudhuria hafla hio ya kihistoria ambapo ilihudhuriwa na wafuasi kutoka wa vyama tofauti vya kisiasa vilivyoshindana katika uchaguzi.

Shein wa chama tawala cha CCM (Chama Cha Mapinduzi) alitangazwa kuwa rais wa Zanzibar baada ya uchaguzi wa jumapili ambapo alimshinda mpinzani wake wa karibu Maalim Seif Sharif Hamad wa chama cha CUF (Civic United Front) kwa kura takriban elfu nne.

Chini ya muafaka walikubaliana kugawana madaraka,na Maalim Seif anatarajiwa kuwa makamu wa rais wa kwanza katika serikali hio. Akitoa hotuba yake baada ya kuapishwa rasmi,rais Shein ameahidi kuendeleza ushirikiano na vyama vyengine visiwani humo.

Raia wengi wa Zanzibar waliojitokeza kupiga kura walisifu hali ya amani iliokuwepo tofauti na chaguzi zilizopita ambapo kulikuwa ghasia na mapigano.