Waziri wa zamani wa Kenya kukutana na Ocampo

William Ruto
Image caption William Ruto

Aliyekuwa waziri wa elimu ya juu nchini Kenya , William Ruto, amewasili mjini The Hague, Uholanzi , kukutana na kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC.

Ruto aliondoka nchini Kenya jana usiku kukutana na mwendesha mashtaka huyo, Luis Moreno Ocampo.

Mkutano huo unafuatia ombi la Bwana Ocampo kwa maafisa wakuu wa serikali ya Kenya, kutoa maelezo zaidi kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi.

Akizungumza katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kabla ya kuondoka, Ruto amesema anapanga kuelezea kile anachofahamu kuhusu matukio ya kabla na baada ya ghasia za mwaka wa 2008.

Ruto amesema huenda wakakutana na Ocampo hii leo au kesho kabla ya kurejea nyumbani siku ya Jumapili. Awali ruto alinukuliwa akisema, atafika katika mahakama hiyo ya ICC ikiwa atahitajika kufanya hivyo.

Ripoti kadhaa za mashirika ya kutetea haki za kibinadamu zimedai Ruto na maafisa wengine wakuu serikalini pamoja na wafanyabiashara walihusika katika kupanga na kufadhili ghasia hizo, madai ambayo wamekanusha.

Mahakama hiyo ya kimataifa ya ICC inafanya uchunguzi wake kuhusu ghasia hizo na imetangaza kuwa itawafungulia mashtaka maafisa 6 wakuu katika serikali ya sasa.

Mashahidi ambao wanakisiwa kuwa na habari muhimu kuhusu waliopanga ghasia hizo wamehamishwa hadi mataifa ya kigeni baada ya kudai kuwa maisha yao yamo hatarini.

Zaidi ya watu 1000 waliuawa kwenye ghasia hizo na maelfu ya wengine kuhama makazi yao.

Ripoti zaidi zinasema kuwa mawaziri wengine wawili wakuu serikalini wanajiandaa kwenda Hague kukutana na Ocampo.