Ruto kuandikisha taarifa kwa ICC leo

William Ruto
Image caption William Ruto

Mwanasiasa mmoja mashuhuri nchini Kenya, William Ruto, anatarajiwa kutoa taarifa rasmi baadaye leo katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC.

Bw Ruto aliwasili mjini The Hague, Uholanzi, hapo jana kukutana na kiongozi wa mashtaka katika mahakama hiyo ya ICC, Luis Moreno Ocampo.

Waziri huyo wa zamani wa Elimu ya Juu, amasema amesafiri kuelezea kile anachofahamu kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi.

Image caption Waziri wa Sheria wa Kenya

Waziri wa sheria wa Kenya Mutula Kilonzo amesema uzito wa kesi hiyo ya ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya, umeanza kujitokeza,''tayari wameshaelewa kwamba huu sio mchezo kwa sababu kuna wale waliopinga kuundwa kwa mahakama maalum nchini Kenya, kuchunguza ghasia hizo wakidhani kwamba mahakama ya ICC itachukua muda mrefu, kama miaka kumi''.

Mahakama hiyo ya uhalifu wa kivita inachunguza mapigano yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 1200, huku wengine wapatao 250,000 wakiachwa bila makao.

Bw Ruto amekanusha kuhusika katika machafuko hayo, japo shirika la kutetea haki za binadamu, linalofadhiliwa na serikali KNHRC imemtuhumu Bw Ruto kuhusika na ghasia hizo.