Man City kukata rufaa kadi ya Balotelli

Meneja wa Manchester City Roberto Mancini amesema watakata rufaa dhidi ya kadi nyekundu aliyooneshwa mshambuliaji wao wa pembeni Mario Balotelli walipocheza na West Brom siku ya Jumapili.

Image caption Mario Balotelli

Balotelli alioneshwa kadi nyekundu moja kwa moja baada ya kuonekana akimpiga Youssuf Mulumbu wakati Manchester City iliposhinda mabao 2-0 katika uwanja wa The Hawthorns.

Meneja huyo wa Manchester City Mancini, anahisi Balotelli hakupaswa kuoneshwa kadi nyekundu, ambayo itamkosesha kucheza mechi siku ya Jumatano dhidi ya mahasimu wao wakubwa Manchester United.

Mancini amesema: "Sikubaliani kabisa na uamuzi wa mwamuzi kumtoa nje. kadi nyekundu ya nini pale?"

Meneja huyo aliongeza kusema: "Alicheza mchezo mzuri, amefunga mabao mawili, lakini kutolewa kwa kadi nyekundu ni jambo lisiloeleweka.

"Nataka kufahamu kwa nini ilikuwa ni kadi ya moja kwa moja nyekundu. Nionavyo haikuwa sahihi na mwamuzi ni lazima atoe maelezo.

"Nimekasirika kwa sababu nilizungumza naye kabla ya mechi, awe makini na mwamuzi. Nilikuwa nataka kumuingiza Adam Johnson badala yake, lakini sikuwa na muda wa kufanya mabadiliko hayo": Aliongeza meneja huyo wa Manchester City.

Ushindi huo muhimu wa Man City umekuja baada ya timu hiyo kupokea vipigo vitatu mfululizo, na umeinua matumaini ya kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao wakijizatiti nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu ya England.

Manchester City katika mchezo huo walikuwa na nahodha wao aliyekuwa amejeruhiwa Carlos Tevez.