Waghana watatu kuwania uchezaji bora

Wachezaji watatu wa Ghana akiwemo mshambuliaji wa Sunderland Asamoah Gyan wameteuliwa kuwania tuzo ya mchezaji bora wa Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf) kwa mwaka 2010.

Image caption Asamoah Gyan

Kiungo Andre Ayew anayecheza soka Ufaransa na Kevin Prince Boateng wa AC Mlian pia majina ni miongoni mwa watakaowania tuzo hiyo.

Watakabiliana na ushindani mgumu kutoka kwa wachezaji wengine ambao wamewahi kushinda tuzo hiyo akiwemo Samuel Eto'o wa Cameroon aliyewahi kushinda mara tatu na washambuliaji wa Chelsea kutoka Ivory Coast, Didier Drogba na Salomon Kalou.

Wachezaji wawili wa Misri Mohamed 'Geddo' Nagy na Ahmed Hassan pia wametajwa katika orodha hiyo.

Wachezaji hao watatu wa Ghana walikuwa chachu ya mafanikio ya Black Stars iliyokuwa nchi pekee ya Afrika kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia mwezi Juni nchini Afrika Kusini.

Gyan na Ayew walikuwemo katika kikosi cha wachezaji vijana wa Ghana waliofika fainali nchini Angola katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwezi wa Januari.

Eto'o, ambaye amewahi kushinda tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika mara tatu mwaka 2003-2005, aliisaidia Inter Milan kushinda ubingwa wa vilabu vya Ulaya mwezi Mei.

Drogba, aliyenyakua tuzo hiyo mwaka 2006 na 2009, alikuwa nguzo kwa klabu ya Chelsea iliyoshinda ubingwa wa ligi ya England mwezi wa Mei.

Wachezaji hao wawili wa Misri wameteuliwa kuwania tuzo hiyo kutokana na mchango wao kwa timu yao ya taifa iliyoshinda Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya sita.

Nagy na Hassan pia wameteluliwa kuwania nafasi ya mchezaji bora wa Afrika katika kundi la bara la Afrika.

Mshambuliaji wa TP Mazembe Dioko Kaluyituka pia ameteuliwa katika kundi hilo kutokana na mchango wake kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutetea ubingwa wa ligi ya vilabu barani Afrika.