Stoke yailaza Birmingham 3-2

Dean Whitehead aliweza kupachika bao muhimu dakika za mwisho lililoipatia timu yake ya Stoke ushindi wa kwanza baada ya kutetereka katika michezo mitano iliyopita, kwenye mpambano uliokuwa wa kukata na shoka dhidi ya Birmingham katika uwanja wa Britannia.

Image caption Wachezaji wa Stoke wakishangilia bao

Robert Huth alikuwa wakwanza kuipatia bao Stoke kabla ya Ricardo Fuller kufunga bao safi baada ya kuwapangua walinzi wa Birmingham na kuachia mkwaju mkali wa mguu wa kushoto.

Mkwaju wa Keith Fahey wa umbali wa yadi 20, ulianza kufufua matumaini ya Birmingham na dakika mbili baadae kidogo Cameron Jerome akasawazisha kwa kichwa.

Lakini bao la Whitehead ambalo lilikuwa rahisi sana, liliipatia ponti tatu muhimu Stoke na kuifanya timu hiyo sasa kuwa na pointi 13 katika nafasi ya 15.